Msaada huo umekabidhiwa Machi 24, 2026 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Shehena hiyo ya mahindi iliwasili jijini Maputo kupitia ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), na kupokelewa na ujumbe wa Serikali ya Msumbiji ulioongozwa na Waziri wa Mipango na Maendeleo, Salim Cripton Valá.
Akikabidhi msaada huo, Waziri Kombo ameeleza kuwa uhusiano wa Tanzania na Msumbiji ni wa kihistoria na kindugu, ulioasisiwa tangu enzi za waasisi wa mataifa hayo mawili, Julius Kambarage Nyerere na Edward Mondlane. Alibainisha kuwa kutokana na uhusiano huo, Rais Samia amemtuma kufikisha msaada huo ili kuwasaidia waathirika wa mafuriko.
“Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Rais Samia anatoa salamu za pole kwa Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, na wananchi wote kufuatia madhila yaliyosababishwa na mafuriko haya, na ameahidi kuwa Tanzania itaendelea kutoa msaada pale utakapohitajika,” amesema Kombo.
Katika ziara hiyo, Waziri Kombo pia amekutana na Waziri Mkuu wa Msumbiji, Maria Belvinda Levy, ambapo walijadili namna ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, hususan katika masuala ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Serikali ya Msumbiji imetoa shukrani kwa Tanzania kwa msaada huo, ikieleza kuwa ni kielelezo cha undugu na ushirikiano wa dhati uliopo kati ya mataifa hayo mawili.







Post a Comment