KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA TAMISEMI YARIDHISHWA NA HATUA YA UJENZI WA BARABARA PWANI


Na: OWM – TAMISEMI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara za Picha ya Ndege – Bokotimiza pamoja na Kongowe – Forest – Yombo, inayotekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Kibaha, mkoani Pwani.


Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kamati hiyo mkoani humo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Frolent Kyombo, amesema mwenendo wa ujenzi wa barabara hizo unaridhisha na kwamba miradi hiyo ni muhimu katika kuunganisha wilaya ya Kibaha na wilaya jirani, jambo litakalorahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa katika mkoa huo.


Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami unaweza kuchukua muda kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, Kamati imeishauri Serikali kutafuta njia ya kuzifanyia ukarabati barabara hizo kwa kiwango cha changalawe kwa haraka ili ziweze kuendelea kupitika kwa urahisi wakati mchakato wa kuzijenga kwa kiwango cha lami ukiendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.


Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, amesema ofisi hiyo imepokea ushauri wa Kamati na tayari imeanza kuufanyia kazi kwa kuielekeza TARURA kuendelea na ukarabati wa barabara hizo kwa kiwango kilichopendekezwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha.


Barabara ya Picha ya Ndege – Bokotimiza ina urefu wa kilometa 7.8, ambapo hadi sasa kipande cha kilometa 0.52 kimejengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, barabara ya Kongowe – Forest – Yombo ina urefu wa kilometa 19.69, ambapo tayari kilometa 0.7 zimejengwa kwa kiwango cha lami.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imehitimisha ziara yake mkoani Pwani kwa kutembelea na kukagua miradi hiyo ya barabara, na inatarajiwa kuendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro tarehe 15 Machi, 2026.

Post a Comment

Previous Post Next Post