KAMATI YA BUNGE UTAWALA KATIBA NA SHERIA YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA KONGANI YA VIWANDA YA BUZWAGI


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, mapema Machi 13, 2026 amepokea Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Damas Ndumbaro katika ziara ya kikazi iliyofanyika katika Kongani Maalum ya Kiuchumi ya Buzwagi iliyopo Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.


Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati wamepata fursa ya kutembelea miundombinu mbalimbali iliyopo ndani ya kongani hiyo pamoja na kushiriki kikao maalum kilicholenga kujadili masuala muhimu ya maendeleo ya kongani hiyo ili iwe kitovu cha ukuaji wa uchumi kwa mkoa na taifa kwa ujumla.


Wajumbe wa kamati hiyo pia wametoa maelekezo, maoni na mapendekezo yao kuhusu namna bora ya kuendeleza kongani hiyo ili kuvutia uwekezaji zaidi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.


Aidha, kamati hiyo imepongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Kampuni ya Barrick pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kwa ushirikiano wao katika kusimamia na kuendeleza kongani hiyo.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Ndumbaro, amesema ni muhimu kwa mamlaka mbalimbali nchini kushirikiana katika kurahisisha uwekezaji badala ya kuwa vikwazo kwa wawekezaji.


Amesema TISEZA inaendelea kufanya kazi nzuri kwa kushirikiana na Wizara ya Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji katika kuhamasisha uwekezaji na kuboresha mazingira ya biashara nchini.


Naye, Dkt. Chaya amebainisha kuwa Serikali itatekeleza agizo la Kamati la kuanzisha Kituo cha Huduma kwa Pamoja (One Stop Center) ili mwekezaji anapofika apate vibali vyote kwa wakati mmoja bila urasimu.


“Tumepokea maelekezo ya kamati ambayo yanatutaka kuhakikisha kwamba sasa tunaanzisha kituo hapa ili kupunguza urasimu kwa wawekezaji wetu watakaokuja hapa ili mwekezaji anapotoka huko akifika hapa apate huduma zote kwa wakati”, amesema Dkt. Chaya.


Dkt. Chaya ameweka wazi malengo makubwa ya kiuchumi ambayo Buzwagi SEZ ni sehemu ya utekelezaji wake ikiwamo Pato la Taifa kufikia Dola za Kimarekani Trilioni Moja ifikapo mwaka 2050, pato la mtu mmoja kufikia wastani wa Dola za Kimarekani 7,000 kwa mwaka.

Post a Comment

Previous Post Next Post