DAR NA PWANI KUPEWA KIPAUMBELE HUDUMA ZA MAJI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuimarisha huduma katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Masanja Kadogosa, amesisitiza umuhimu wa kudhibiti upotevu wa maji na kukamilisha miradi ya kimkakati ili kuendana na kasi ya ukuaji wa makazi na uchumi katika maeneo hayo ambayo ni vitovu vya biashara na viwanda.


Mhe. Kadogosa amebainisha kuwa Dar es Salaam na Pwani ni maeneo muhimu yanayohitaji mikakati mahususi ya usimamizi wa huduma ili kukidhi mahitaji ya mataifa yanayotumia lango la biashara la Tanzania.


Ameitaka DAWASA kubuni vyanzo vipya vya maji vitakavyohakikisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa uhakika, jambo ambalo ni nguzo kuu katika kukuza uchumi wa viwanda na ustawi wa wananchi nchini.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango wa DAWASA, Ndugu Paul Sulley, ameeleza kuwa mamlaka inatekeleza miradi mbalimbali mikubwa ukiwemo wa Bwawa la Kidunda na upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Chini.


Aidha, amebainisha maandalizi ya mradi wa kutoa maji Mto Rufiji na ununuzi wa pampu za visima vya Kimbiji, hatua ambazo kwa pamoja zimepangwa kuleta suluhu ya kudumu ya upatikanaji wa maji safi katika mikoa hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post