WAJUMBE WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA TAMISEMI WASHAURI UPANUZI WA ENEO LA STENDI MIKUM


Kamati ya kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imeishauri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM- TAMISEMI) kutoa maelekezo mahususi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro juu ya eneo la ujenzi wa kituo cha mabasi katika mji wa Mikumi mkoani humo.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Frolent Kyombo ametoa mapendekezo hayo kwa niaba ya kamati wakati wa majumuisho ya ziara ya kamati hiyo baada ya kutembelea na kukagua eneo inapotarajiwa kujengwa stendi ya mbasi katika mji wa Mikumi pamoja na kukagua ujenzi wa barabara zenye urefu wa Kilomita 1.5 zinazojengwa kwa kiwango cha zege katika mji huo.


Mhe. Kyombo amesema “Wajumbe wanashauri pamoja na OWM - TAMISEMI kutoa maelekezo mahususi juu ya ukubwa wa eneo la kujengwa kwa kituo hicho cha mabasi, lakini pia tunaishauri Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa itafute fedha kutoka mapato ya ndani au kwa kukopa lakini ianze kutekeleza ujenzi wa mradi huu, fedha kutoka Serikali kuu itawakutia njiani”.


Kadhalika amesema kamati imeshauri Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuwalipa fidia wananchi wanaozunguka eneo la ujenzi wa stendi hiyo lenye ukubwa wa hekari 1.6 ili kutanua eneo hilo na kuondoa migongano baina ya Serikali na wananchi.


Naibu Waziri OWM-TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, ametumia fursa hiyo kuzitaka halmashauri nchini kuzingatia mwenendo wa ongezeko la watu wakati wa kupanga na kujenga miradi ya maendeleo ili miundombinu inayojengwa iweze kukidhi mahitaji ya wananchi kwa muda mrefu.


Ujenzi wa mradi wa stendi ya mabasi ya kisasa katika mji wa Mikumi unatarajiwa kuboresha ufanisi wa huduma za usafiri na kuchochea ongezeko la mapato ya halmashauri kutoka Shilingi Milioni 226.7 hadi Shilingi Bilioni 1.012 kwa mwaka, kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazofanyika katika kituo hicho cha mabasi.

Post a Comment

Previous Post Next Post