KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UWEKEZAJI WA MRADI WA FARU

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeeleza kuridhishwa na uwekezaji uliofanywa na Serikali katika mradi wa Faru, ambao umechangia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi iliyopo Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.


Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo mara baada ya kutembelea na kukagua mradi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mary Masanja, amesema mradi huo ni wa kujivunia kwa kuwa umeonesha matokeo chanya kwa kuongeza kwa kasi idadi ya watalii pamoja na mapato ya hifadhi hiyo.


Mhe. Masanja amebainisha kuwa mafanikio ya mradi huo yanatokana na juhudi za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha sekta ya utalii kwa kuongeza mazao mapya ya utalii, kuongeza siku za wageni kukaa nchini pamoja na kuinua sekta za maliasili na utalii kwa ujumla.


Aidha, Mhe. Masanja ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa usimamizi mzuri wa mradi huo, pamoja na kuwapongeza askari wanaolinda wanyamapori kwa uzalendo na ujasiri wao katika kuwalinda faru ambao walikuwa hatarini kutoweka.


Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mbunge wa Jimbo la Hanang Asia Halamga amesema.


Akieleza madhumuni ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Hassan Abbasi, amesema mradi huo unalenga kuongeza juhudi za uhifadhi wa mnyama faru ambaye alikuwa hatarini kutoweka, kuvutia watalii zaidi katika hifadhi hiyo, kutengeneza ajira hususan kwa vijana, pamoja na kuchangia zaidi katika pato la taifa.


Dkt. Abbasi pia ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ili kufurahia urithi adhimu wa maliasili uliopo.


Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, ameishukuru Kamati hiyo kwa ziara waliyofanya katika hifadhi hiyo kukagua na kujionea maendeleo ya mradi huo. Amesema Wizara yake itafanyia kazi kwa haraka maoni, ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post