Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam imefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 64 raia wa Malawi katika operesheni maalumu zinazoendelea mkoani humo za kudhibiti uhamiaji haramu na kuimarisha usalama.
Zoezi hilo la ukamataji lilifanyika tarehe 14 Juni 2026 katika maeneo ya Mwananyamala, Kijitonyama, Mikocheni B na Mikocheni Msikitini, Wilaya ya Kinondoni. Wahamiaji hao walibainika kuingia na kuishi nchini bila kuwa na vibali halali, jambo ambalo ni kinyume na Sheria za Uhamiaji za Tanzania.
Akizungumza kuhusu operesheni hiyo, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji (SACI) Vincent Haule, amewapongeza wananchi kwa ushirikiano wanaouonyesha kwa Idara ya Uhamiaji katika kufichua wahamiaji haramu na kusaidia kuhakikisha mkoa unaendelea kuwa salama.
SACI Haule amesema ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola ni nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya uhamiaji haramu na uhalifu mwingine unaoweza kuhatarisha usalama wa jamii.
Aidha, amewataka Maafisa Uhamiaji wa wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi ili kudhibiti na kukomesha wimbi la wahamiaji haramu pamoja na kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa.
Idara ya Uhamiaji inaendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini uwepo wa watu wanaoshukiwa kuingia au kuishi nchini kinyume na sheria, ili kuimarisha usalama na kulinda maslahi ya Taifa.
#Uhamiajiusalamanamaendeleo
#Mjuejiraniyako


Post a Comment