Mafunzo hayo yalifanyika Juni 13, 2026 na kuendeshwa na Mkuu wa Kitengo cha Maafa na Majanga kutoka Kamisheni ya Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi Makao Makuu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Deogratius Massawe akishirikiana na wakufunzi Mrakibu wa Polisi SP Msafiri Shogholo, Konstebo Edward Mahundi, Konstebo Davis Mbuda na Konstebo Madina Mwarabu.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, ASP Shogholo alisema kuwa lengo ni kuwajengea askari uelewa wa kina kuhusu namna ya kukabiliana na matukio ya majanga kwa weledi, haraka na usalama ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi na mali zao.
Alieleza kuwa askari wanapaswa kutambua wajibu wao katika hatua zote za usimamizi wa majanga, ikiwemo maandalizi, mwitikio wa haraka, uokoaji na urejeshaji wa hali ya kawaida baada ya tukio kutokea.
Aidha, washiriki walikumbushwa umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kuzingatia usalama wao binafsi kabla ya kuanza shughuli za uokoaji, hususan katika matukio yanayohusisha ajali za magari yanayobeba kemikali hatarishi, ambapo hatua za kitaalamu zinapaswa kufuatwa ili kuepusha madhara zaidi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi za kuendelea kuimarisha uwezo wa watendaji wake katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama na kibinadamu zinazoweza kujitokeza wakati wowote, kwa lengo la kulinda maisha ya wananchi na mali zao.






Post a Comment