▪️Awataka waliopewa dhamana ya usimamizi wazingatie misingi ya utawala bora
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameziagiza Mamlaka, Taasisi na Wadau wote waliopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 wabadilike na wahakikishe wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na utawala wa sheria ili kufikia malengo na shabaha zilizoainishwa katika Sera hiyo.
Amesema taarifa za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma zinaonesha kuwa changamoto katika ununuzi wa umma siyo Sera, Sheria wala Kanuni, bali ni waliopewa dhamana ya kusimamia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za Ununuzi.
Waziri Mkuu amesema kuwa sehemu kubwa ya shughuli za ununuzi zinaathiriwa zaidi na mitazamo, hulka na tabia za wataalamu na watendaji ikilinganishwa na upungufu wa masuala ya kisera na kisheria, hivyo amewataka wadau wa Sekta Binafsi waweke mikakati ya kuimarisha mifumo ya ushirikiano na sekta ya umma ili kunufaika kikamilifu na fursa zilizobainishwa katika Sera hiyo.
Ametoa maagizo hayo (Jumatano, Aprili 8, 2026) alipozindua Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. “Leo tunaweka alama muhimu katika historia ya usimamizi wa mali na rasilimali za Taifa letu”.
Amesema hatua hiyo ya kisera inalenga kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za ajira na kipato, pamoja na kujenga uchumi jumuishi na shindani unaomilikiwa na Watanzania walio wengi. “Kwa ujumla, fursa hizi zinalenga kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza uzalishaji wa bidhaa, Utoaji wa huduma pamoja na kukuza uwiano wa upatikanaji wa bidhaa na huduma”.
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa mara ya kwanza, Tanzania inakuwa na mwongozo mmoja wa kisera unaounganisha na kufungamanisha mtazamo wa kimfumo na hatua zote muhimu katika mnyororo wa ugavi, kuanzia ununuzi, ugomboaji, upokeaji, urejeshaji, uhifadhi, matumizi, usambazaji hadi uondoshaji wa mali za umma”.
Taarifa za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma zinaonesha kuwa changamoto katika ununuzi wa umma siyo Sera, Sheria wala Kanuni, bali ni waliopewa dhamana ya kusimamia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za Ununuzi-Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba
Amesema hayo alipozindua Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Post a Comment