RAIS DKT. SAMIA AKUTANA NA WAGOMBEA 16 WA URAIS 2025 IKULU, SIASA ZA KUVUMILIANA ZAHIMIZWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Wagombea wa Nafasi ya Urais na Wagombea Wenza kutoka vyama vya Siasa 16 vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2025. Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 31 Machi, 2026.


Wagombea wa nafasi ya Urais kutoka vyama 16 vya siasa nchini vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, wametoa mwito wa kuimarishwa kwa siasa za staha, uvumilivu, na kuheshimiana miongoni mwa wadau wa kisiasa kama njia pekee ya kulinda amani na kukuza uchumi wa taifa.


Msisitizo huo umetolewa, Machi 31, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wagombea hao walipomtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia maombi yao ya kufanya majadiliano ya pamoja kuhusu mustakabali wa nchi baada ya kukamilika kwa uchaguzi.


Katika mazungumzo hayo ya aina yake, viongozi hao wameeleza kuwa taifa linahitaji utamaduni wa mazungumzo ya mara kwa mara ili kushughulikia changamoto za kitaifa kwa njia ya amani. Walisisitiza kuwa siasa zisizo na staha huleta mpasuko, wakati siasa za uvumilivu hujenga uaminifu ambao ni kichocheo cha maendeleo endelevu.


“Majadiliano hayo pia yaligusia umuhimu wa kuendeleza maadili ya uongozi, uwajibikaji na siasa zenye staha, kama msingi wa kujenga Taifa lenye utulivu wa kisiasa na maendeleo endelevu”, imeeleza taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.


Mbali na mivutano ya kisiasa, wagombea hao wamemshauri Rais Samia kuimarisha demokrasia jumuishi kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Wamebainisha kuwa wananchi wanapaswa kuona viongozi wao wakishirikiana katika masuala ya kitaifa ili kuondoa hofu na kuongeza mshikamano baada ya kinyang'anyiro cha kura kukamilika.


“Sambamba na hilo, walielezea umuhimu wa kuimarisha utamaduni wa uvumilivu wa kisiasa, kuheshimiana na kujenga uaminifu miongoni mwa wadau wa kisiasa, kama njia ya kuendelea kudumisha utulivu wa nchi”, imeeleza taarifa hiyo.


#KaziNaUtuTunasongaMbele

#TabasamuLaUtu

#MaendeleoEndelevu

#DiplomasiaYaKiuchumi

Post a Comment

Previous Post Next Post