WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa tasnia ya mazao ya bustani siyo tu sehemu ya sekta ya kilimo, bali ni sekta ya kimkakati ya biashara ya kimataifa inayounganisha Tanzania na Masoko ya Dunia.
Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu huo, Serikali ya Tanzania imeendelea kutoa ruzuku ya pembejeo iliyosaidia kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya bustani kutoka tani milioni 7. 5 kwa mwaka 2023/2024 hadi kufikia tani milioni 9. 7 kwa mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 30.2.
Amesema hayo (Jumatano, Aprili 22, 2026) alipozindua maandalizi kuelekea Jukwaa la Hotikacha la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji (Hortilogistica Africa 2026) hafla hiyo imefanyika kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Jukwaa la Kilimo wa Dkt. John Samwel Malecela Nzuguni jijini Dodoma. Jukwaa hilo linatarajiwa kufanyika jijini Arusha, Novemba 08 hadi 10, Mwaka huu.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha Tanzania inaendelea inakuwa Kitovu cha Biashara ya Mazao ya bustani Afrika na lango la Masoko ya Kimataifa, Serikali imeendelea kupanua wigo wa masoko ya Kimataifa ambapo kwa sasa mauzo ya parachichi, mbogamboga, maua na viungo vinavyozalishwa nchini yameongezeka kwa kasi hususan katika Masoko ya Ulaya na Mashariki ya Kati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa wakulima nchini kuzingatia ubora na viwango vinavyokubalika kimataifa ili kuleta ushindani wa bidhaa za Kitanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa, “Biashara ni ubora, bidhaa ikiwa na ubora haiwezi kukosa soko”-Alisisitiza Dkt. Mwigulu
Mheshimiwa Waziri Mkuu aliongoza harambee iliyolenga kukusanya shilingi bilioni 2 katika awamu ya kwanza. Hata hivyo, kiasi kilichopatikana kilivuka lengo hilo na kufikia shilingi bilioni 2.59. Kwa ujumla, ifikapo mwezi Novemba, jumla ya shilingi bilioni 6 inatarajiwa kukusanywa.


Post a Comment