WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali itachukua hatua kali ikiwemo kufilisiwa kwa yeyote anatakayebainika kuhujumu wakulima kwa kuwauzia pembejeo zisizokuwa na ubora zikiwemo mbegu.
Ameyasema hayo, Jumapili, Machi 08, 2026 alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Laela A wilayani Sumbawanga, Rukwa. Amesisitiza kuwa watu hawatovumiliwa kwa kuwa wana lengo la kuliingiza Taifa katika njaa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Sylvia Sigula kuishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku ya pembejeo ila ameiomba Serikali kuwatatulia changamoto ya kuuziwa mbegu zisizokuwa na ubora jambo linalosababisha wakulima kupata hasara kwani kilimo ndio uchumi wa Rukwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema wizara amekuwa ikifanya uchunguzi na kuchukua hatua pale inapobaini kuwepo kwa pembejeo zisizokuwa na ubora na tayari kuna mtu mmoja amekamatwa mkoani humo.
Vilevile, Naibu Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuwaelimisha wananchi kuwa mbegu na mbolea za ruzuku zinazotolewa na Serikali zinakuwa na namba za utambuzi ambazo ukiingiza kwenye namba *148*52# itaeleza kama ni halali, hivyo amewasisitiza wakulima kuendelea kuwa makini.
Awali, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania kwamba mambo yote yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi yatatekelezwa kwa vitendo kwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mtu wa matokeo na akisema jambo anatekeleza.
“Watu wa Rukwa ni mashahidi kutokana na utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yenu ikiwemo ujenzi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya na shule za msingi, sekondari na za amali, hili ni jambo kubwa linaloleta heshima kwa nchi.”
*WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA SOKO LA KISASA LA MAZAO KANONDO-RUKWA.*
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, Machi 8, 2026 ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Soko la Kisasa la Mazao Kanondo lililopo Sumbawanga mkoani Rukwa.
Ujenzi wa soko hilo unatekelezwa kupitia Mradi wa TACTIC kwa gharama ya shilingi bilioni 7.3, na hadi sasa umefikia asilimia 82 ya utekelezaji.
Soko hilo linatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha biashara ya mazao, likiwaunganisha wakulima, wanunuzi wakubwa, wasafirishaji na wawekezaji, hatua itakayopanua mtandao wa biashara na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wa Rukwa na maeneo jirani.
*WAZIRI MKUU AKAGUA UKARABATI WA UWANJA WA NDEGE WA SUMBAWANGA*
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba Machi 08, 2026 amekagua maendeleo ya ukarabati na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga uliopo mkoani Rukwa.
Mradi huo ulianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa gharama ya shilingi bilioni 60.1 na hadi sasa umefikia asilimia 96 ya utekelezaji.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Dkt. Mwigulu amewapongeza wananchi wa Rukwa kwa kupata uwanja wa ndege wa kisasa kwa kuwa maendeleo hayo yanaonesha mabadiliko makubwa ya mkoa huo.
Amesema kuwa kwasasa Rukwa siyo ile ya zamani bali ni Rukwa ya kisasa na ya viwango, inayokwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya taifa.
Aidha, amesema miradi ya aina hiyo ndiyo mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inajivunia kwa kuwekeza katika miradi ya maendeleo yenye tija na inayoacha alama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Ukarabati na upanuzi wa uwanja huo unatarajiwa kuimarisha huduma za usafiri wa anga katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameanza ziara ya kikazi katika mkoa wa Rukwa ambapo atakagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.


Post a Comment