WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Machi 2, 2026 amekagua Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Kilutheri ya Haydom iliyopo Wilaya ya Mbulu, Mkoa wa Manyara, ambalo ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 6.3.
Mradi huo unalenga kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za mama na mtoto kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya tiba na usalama wa wagonjwa na hatimaye kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaohitaji kupatiwa huduma hiyo.
Hospitali hiyo ya Kanisa imeendelea kuwa mdau muhimu wa Serikali katika kuboresha huduma za afya ya jamii, ikiwemo utoaji wa huduma za rufaa na kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na mikoa jirani.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Dkt. Mwigulu amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua kazi kubwa inayofanywa na madhehebu ya dini ikiwemo Kanisa la Kilutheri katika kuchangia ustawi wa jamii.
“Serikali iliona umuhimu wa taasisi zinazofanya kazi hii zipate misamaha ya kodi kwasababu zinashiriki kuimarisha huduma za kijamii, pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anatambua kazi kubwa inayofanywa na watumishi katika sekta ya afya ikiwemo wa hapa Haydom kwa kuwa mnafanya kazi kubwa ya kuokoa uhai wa watanzania.”
*WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA BARABARA YA MBULU – GARBABI (KM 25)*
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amekagua mradi wa ujenzi wa barabara kipande cha Mbulu – Garbabi (km 25), ambacho ni sehemu ya barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (km 389) inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Mradi huo unaotekelezwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) unalenga kuboresha mawasiliano ya barabara, kuimarisha usafirishaji wa watu na bidhaa, na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo husika.
Hadi sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 41.7, ambapo jumla ya shilingi bilioni 36.3 zitatumika kukamilisha ujenzi. Mpaka sasa malipo ya shilingi bilioni 12.5 tayari yameshafanyika.


Post a Comment