DKT. TULIA APELEKA MILIONI 41 UJENZI WA MABWENI ITEZI SEKONDARI

Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson amepeleka shilingi milioni 41 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mabweni katika Shule ya Sekondari Itezi, jijini Mbeya.


Fedha hizo zimetolewa kupitia Mfuko wa Jimbo la Uyole kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, hususan wa kike wa kidato cha nne watakaonufaika na ujenzi wa bweni jipya. Ujenzi huo unatarajiwa kuwasaidia wanafunzi hao kupata utulivu na muda wa kutosha kujiandaa na mitihani yao ya taifa.


Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo, Dkt. Tulia amesema kiasi hicho kitawekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya shule ili kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika matumizi. Ameitaka bodi ya shule pamoja na viongozi wa Kata ya Itezi kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mradi huo ili thamani ya fedha ionekane.


“Ni wajibu wetu kuhakikisha watoto wetu wanapata mazingira bora ya kusoma. Nitaendelea kutafuta fedha zaidi ili kukamilisha ujenzi huu kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa,” amesisitiza Dkt. Tulia.


Mbali na mradi huo, Dkt. Tulia amesema mpango wa sasa katika Jimbo la Uyole ni kuhakikisha shule zote za sekondari zinakuwa na madarasa ya kidato cha tano na sita, hatua itakayopanua fursa za elimu ya juu kwa wanafunzi wa jimbo hilo na kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta masomo ya juu ya sekondari.

Post a Comment

Previous Post Next Post