Bw. Onanga-Anyanga ametoa pongezi hizo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya mwanzo ya mazungumzo yake na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa kitaifa.
Mjumbe huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi kwa lengo la kufanya mashauriano na Serikali na wadau wengine wa kitaifa kuhusu hali ya kisiasa nchini, pamoja na kujadili namna Umoja wa Mataifa unavyoweza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kusimamia mageuzi na kuendeleza umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia maridhiano jumuishi.Aidha, amempongeza Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha utulivu na uongozi makini katika kipindi hicho kigumu kwa taifa. Amekaribisha pia uamuzi wa Serikali wa kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025
Bw. Onanga-Anyanga aliipongeza Tume hiyo inayoongozwa na Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu Mstaafu kwa kazi yake nzuri yenye kubeba uzito na ubobezi na viwango vya hali ya juu na ya kuigwa kimataifa. Ameeleza pia kuwa muundo wa Tume hiyo unaojumuisha wajumbe kutoka kada mbalimbali umeongeza ubora na uhuru wa kazi yake.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kurejesha imani ya wananchi na kudumisha utulivu baada ya matukio hayo, pamoja na hekima na utulivu uliotumika katika kushughulikia changamoto zilizojitokeza wakati wa kipindi cha uchaguzi.




Post a Comment