Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuongeza juhudi za kudhibiti upotevu wa maji na kuimarisha huduma katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Maelekezo hayo yametolewa baada ya kamati hiyo kupokea na kujadili taarifa ya mamlaka hiyo katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa PIC, Masanja Kadogosa, amesema eneo la huduma la DAWASA linaendelea kukua kwa kasi kutokana na ongezeko la makazi na shughuli za kiuchumi, hivyo kuna umuhimu wa kukamilisha miradi ya maji safi pamoja na kubuni vyanzo vipya vya maji ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma unakuwa wa uhakika.
Amesema kuwa Dar es Salaam ni kitovu cha biashara na lango la uchumi kwa mataifa mengi, huku Pwani ikiwa kitovu cha shughuli nyingi za viwanda, hali inayohitaji kuwepo kwa mikakati madhubuti ya usimamizi wa huduma za maji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Kadogosa ameisisitiza DAWASA kusimamia kwa karibu miradi ya kimkakati na kuhakikisha inapunguza kwa kiwango kikubwa upotevu wa maji katika mtandao wake.
Awali akiwasilisha taarifa ya mamlaka hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mipango, Tafiti na Ufuatiliaji, Paul Sulley, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma.
Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji wa Bwawa la Kidunda, upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini, ununuzi wa pampu kubwa kwa ajili ya visima virefu vya Kimbiji pamoja na maandalizi ya mradi wa kuvuta maji kutoka Mto Rufiji, ambayo kwa pamoja inatarajiwa kuongeza uhakika wa huduma ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Post a Comment