Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, iliyofanyika Kilimani, Chato mkoani Geita.
Akitoa salamu za Serikali, Makamu wa Rais amesema ili kumuezi Hayati Magufuli kwa vitendo ni vema kila Mtanzania kujifunza wito kwa kujitoa na kufanya kazi kwa bidii. Amesema Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliyejitambulisha kwa Falsafa yake ya “Hapa Kazi tu”, alitaka kila mtu kujituma na kutoa mchango wake kwa Taifa kwa njia ya kazi. Aliamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kuondoa umaskini, katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, kaya na hata Taifa kwa ujumla.
Makamu wa Rais amesema katika uongozi, funzo kutoka kwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ni ujasiri na uthubutu wake katika kufanya maamuzi magumu na yenye manufaa kwa Taifa. Ameongeza kwamba alifundisha umuhimu wa kuwajibika na kusimamia misingi ya haki na usawa katika kuwahudumia wananchi wote, pia hakuyumbishwa katika kupiga vita uzembe na rushwa.
Halidhalika, Makamu wa Rais ameongeza kwamba, Hayati Magufuli, alifundisha kuwa hatima ya Tanzania na Afrika kwa ujumla iko mikononi mwa Watanzania na Waafrika wenyewe. Akisisitiza ulinzi na matumizi ya utajiri mkubwa wa rasilimali zilizopo, kwani zinaweza kuwatoa wananchi katika umaskini. Amesema, Hayati Magufuli aliamini kuwa wajibu wa kutatua matatizo ya nchi ya kijamii, kisiasa au kiuchumi yako mikononi mwa Watanzania wenyewe.
Makamu wa Rais amesema katika uhai wake, Hayati Dkt. John Magufuli aliwagusa wengi kupitia utumishi na uongozi wake uliotukuka. Pamoja na mambo mengine, Mwenyezi Mungu alimjalia Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kipawa cha uongozi na uwezo mkubwa wa kunena na kutenda yote aliyoyaamini kuwa ya manufaa kwa Taifa na watu wake. Kila siku ya maisha yake ilijaa mafunzo kwa kila aliyemwona au kufanya naye kazi. Ameongeza kwamba, maisha yake yalikuwa ni darasa zuri kwa viongozi, na kupitia uongozi wake aliweza kulea na kuinua viongozi wapya wengi, hasa vijana.


Post a Comment