MBUNGE SAMIRA AMOUR AKABIDHI MAHITAJI KATIKA SHULE ZA MAHITAJI MAALUMU - BIHARAMULO

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Mhe. Samira Amour Khalfan ametembelea shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Wilaya ya Biharamulo na kupeleka mahitaji katika Shule ya Msingi Biharamulo A pamoja na Shule ya Iyangamulilo iliyopo Kata ya Nyatakara.


Samira ametembelea shule hizo tarehe 25 Februari 2026 ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika wilaya zote za Mkoa wa Kagera ya kuzitembelea shule na vituo vyenye watoto na wanafunzi wenye mahitaji maalum katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan pamoja na Kwaresma.


Katika ziara hiyo, Mbunge Samira amekabidhi mahitaji muhimu ikiwemo mchele, sukari, mafuta ya kupikia, unga wa ugali, sabuni za kufulia na kuogea, mafuta ya kujipaka, dawa za meno na miswaki, taulo za kike pamoja na vinywaji kama juisi, soda na biskuti.


Aidha, Samira ametoa shilingi 180,000 kwa ajili ya kununua mahitaji ya mtoto mwenye ualbino ili aweze kuanza masomo, na ameeleza kuwa dhamira yake ni kurejesha tabasamu na matumaini kwa watoto na wanafunzi ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea tabasamu wananchi na kuonesha upendo, kuthaminiwa na kupewa furaha.


Akizungumza Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Biharamulo A, Mwl Julius Magezi amemshukuru Samira pamoja na wadau wengine ambao wamekuwa na moyo wa kuwakumbuka wanafunzi wenye mahitaji maalum huku akieleza changamoto za shule ambazo ni pamoja na upungufu wa walimu, vifaa vya michezo, vifaa vya kula na huduma nyingine muhimu kama mavazi.

Post a Comment

Previous Post Next Post