Baada ya kupata taarifa za wasamalia wema kuhusu uwepo wa mtoto aliyepata ajali mbaya ya kuungua moto toka mwaka Jana 2025 mwezi Novemba lakini hadi sasa hakuna matibabu yoyote ya kueleweka anayopatiwa zaidi ya kufanyiwa maombi tu ndani, ndipo leo Alhamisi Februari 26, 2025 Afisa Tarafa ya Katerero Ndugu Bwanku M Bwanku akiongozana na Mtendaji wa Kijiji cha Buganguzi, Kata ya Bujugo Ndugu Anthony Babolio, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata Ndugu Mdashiru Hamoud na Mjumbe mmoja wa Serikali ya Kijiji walifika kwenye familia hiyo kujua ukweli wa jambo hilo.
Baada ya kufika kwenye familia hiyo walimkuta mtoto huyo mguu ukiwa umeanza kuoza na ukianza kupinda huku Mama wa mtoto akithibitisha hawajawahi kumpeleka hospitali zaidi ya kumfanyia maombi ndani na dawa za kienyeji na chache za kununua madukani bila ya kumpeleka kupata matibabu ya kueleweka ya kitaalamu hospitali.
Wote walisikitishwa kwa mtoto huyo anayepitia maumivu makali ya kidonda cha kutisha kutopelekwa hospitali, ndipo Afisa Tarafa Bwanku na Watendaji walivyochukua uamuzi wa kumchukua kumpeleka zahanati ya Bujugo na kisha Hospitali ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera (Bujunangoma) kwa matibabu zaidi badala ya mtoto huyo kuendelea kubaki ndani akifanyiwa maombi, mguu ukiwa na dalili ya kuoza pamoja na mtoto huyo kuwa na hatari ya kupata ulemavu wa kudumu kwa kutopata matibabu stahiki ya kitaalamu hospitali mapema.



Post a Comment