Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeeleza kutoridhishwa kwake na mwenendo wa uandishi wa baadhi ya waandishi na mabloga wanaochanganya michakato ya uteuzi ndani ya vyama vya siasa na matangazo rasmi ya uchaguzi.
Akizungumza katika mkutano na wazalishaji wa maudhui mtandaoni leo Agosti 3, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, amesema kuwa ni INEC pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi pamoja na orodha ya wagombea.
"Tunashangaa kusikia baadhi ya vyombo vya habari vikisema fulani amepita bila kupingwa, au fulani ameteuliwa kuwa mgombea ubunge wa jimbo fulani, hivi kweli tumeshafanya uchaguzi? Hiyo ni michakato ya ndani ya vyama ya kufanya mapendekezo," amesema Kailima.
Ameongeza kuwa INEC itatangaza orodha ya wagombea urais, ubunge na udiwani baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa. Kuhusu wagombea wa viti maalum, ameeleza kuwa watatangazwa baada ya uchaguzi wa ubunge kukamilika na tume kufanya mahesabu ya asilimia.
"Ni muhimu kwa waandishi na mabloga kutenganisha habari za michakato ya ndani ya vyama na zile za uchaguzi, kwani ubunge hutangazwa na INEC," amesisitiza Kailima.
Mkurugenzi huyo pia amefafanua kuwa jukumu la wakala katika uchaguzi si kulinda kura, bali ni kuangalia maslahi ya mgombea anayemwakilisha.
Alisema kuwa Tume imejipanga kushirikiana na vyombo vya habari katika mchakato mzima wa uchaguzi ili kuweka wazi na kuhakikisha kunakuwepo na uwazi na ushirikiano.
Naye Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele, amewataka wazalishaji wa maudhui mtandaoni kuhakikisha kuwa taarifa za uchaguzi wanazoziweka kwenye kurasa zao za mitandao ni za kweli na zisizokuwa na chembe ya upotoshaji.
Akifungua Mkutano wa Kitaifa baina ya INEC na Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni, Jaji Mwambegele ameeleza kwamba ukosefu wa umakini katika utoaji wa habari wakati wa uchaguzi mkuu unaweza kuharibu na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.
“Ni ukweli kwamba mitandao hasa ya kijamii imekuwa ni chanzo muhimu cha habari kutokana na kuwa taarifa zinazochakatwa kwenye mitandao zinapatikana kwa urahisi na kwa haraka hiyo basi ni muhimu kuhakikisha habari hizo zinakuwa ni za kweli,” amesema Jaji Mwambegele.
Jaji Mwambegela pia, amewaasa Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni kuepuka matumizi mabaya ya Akili Unde (AI) ambayo inatumiwa na baadhi ya watu wenye nia ovu kusambaza habari za upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii.
Kuhusiana na madai ya kuwa idadi ya wapiga kura walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la kupiga kura inawezekana kuwa si sahihi kutokana na uwezekano wa kuwapo watu waliokufa kwenye daftari hilo Jaji Mwambegele amesema;
“Nikweli huenda kukawa na watu waliokufa kwenye daftari la wapiga kura iwapo hatujapata taarifa za mpiga kura aliyepoteza maisha lakini tukipata taarifa hiyo tutamuondoa, ila hata hivyo hakuna mtu aliyekufa anaweza kupiga kura hivyo uwepo wao unajaza nafasi tu hauathiri upigaji kura,” alisema Jaji Mwambegele.
Post a Comment