Wakati Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) ikiufungua rasmi mfumo wa usajili wa Waandishi wa Habari wa https://taihabari.go.tz ili kuomba kuthibitishwa na kupatiwa Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Cards) Mwenyekiti wa Bodi hiyo Ndg. Tido Mhando amewaonya wenye nia ya kutumia vyeti visivyo halali wakati wa kujaza taarifa zao.
Mhando alitoa tahadhali hiyo tarehe 19 Mei, 2025 wakati akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari katika ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam.
“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, Bodi hii itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wa habari wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya kidijiitali (digital Press Card). Maombi ya ithibati Press Cards yatafanyika kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari”, alisema.
Mhando alisema mahitaji muhimu wakati wa kujaza taarifa katika mfumo huo kuwa ni pamoja na namba ya simu na barua pepe vinavyofanya kazi, picha ndogo (passport size) iliyoskaniwa barua ya utambulisho kutoka taasisi anayotoka au anakopeleka kazi zake ikiwa ni mwandishi wa kujitegemea (Freelancer), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na ada ya ithibati shilingi Elfu Hamsini (50,000).
“Mahitaji mengine ni vyeti vya elimu vilivyoskaniwa kwa mfumo wa PDF na kuthibitishwa na Mamlaka husika (kama chuo kikuu vithibitishwe na TCU na kama ni vyuo vya kati vithibitishwe na NACTVET), na katika hili nisisitize tafadhali sana usiweke cheti ‘feki’ jambo hilo linakiuka siyo tu linakiuka maadili ya taaluma habari, bali pia ni makosa yanatakayodhibitiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi,” alisema Mhando.
Post a Comment