WABUNGE WAPONGEZA ONGEZEKO LA IDADI YA WATALII NA MAPATO NCHINI

                    Na Kassim Nyaki, Dodoma


Wabunge wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada kubwa za kutangaza vivutio vya utalii, ambazo zimesaidia kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia 2,141,895 mwaka 2024, huku watalii wa ndani wakiongezeka kutoka 788,933 hadi 3,218,352 katika kipindi hicho.


Kwa upande wa maduhuli ya Serikali yametajwa kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 397.42 Mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 901.08 Mwaka 2023/2024. Aidha mwaka wa Fedha 2024/2025 kuanzia Julai 2024, hadi kufikia Aprili 2025, Wizara imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 912.90 sawa na asilimia 94.2 ya lengo la makusanyo, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko wakati wowote kuwahi kupatikana katika historia ya sekta hii


Pongezi hizo zimetolewa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii 2025/26 iliyowasilishwa na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, ambaye ameomba Bunge liidhinishe Sh. bilioni 359.98.


Akichangia, Mbunge wa Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi, ameipongeza Wizara, taasisi zake za uhifadhi, na wadau wa utalii kwa kazi kubwa ya kuitangaza nchi kimataifa na hivyo kuchangia ongezeko hilo la watalii.


“Tuendelee na mpango wa kutangaza vivutio vya utalii katika nchi za Uarabuni, Japan, Ufaransa, India, na Australia. Ikiwezekana, tutengeneze filamu za utalii kwa lugha za nchi hizo. Tuzitumie pia mashirika ya ndege, vyombo vya habari vya kimataifa, ligi maarufu za mpira duniani, na watu maarufu duniani kutangaza vivutio vyetu. Pia tuendelee kushiriki katika maonesho ya kimataifa kama ITB, ITN ya Ufaransa, na EAC Tourism Expo,” amesema Prof. Ndakidemi.


Naye, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo Mnzava, ameshauri Serikali kuzipa taasisi za uhifadhi uwezo wa kukusanya mapato yatokanayo na utalii na uhifadhi ili kusaidia kuboresha miundombinu ya utalii, kujenga vituo vya askari, na kuweka uzio wa umeme kwenye mipaka ya hifadhi na kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post