Video- KWAGILWA AAGIZA VIBALI VYA USAFISHAJI WA MTO MSIMBAZI VIPITIWE UPYA

Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira,Mhe. Reuben Kwagilwa, ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Bonde la Wami/Ruvu pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kufanya upya mapitio ya vibali vinavyotolewa kwa ajili ya usafishaji wa Mto Msimbazi ili kuhakikisha shughuli hizo hazisababishi uharibifu wa mazingira.


Maelekezo hayo ameyatoa wakati wa ziara ya kukagua hali ya mazingira katika maeneo yanayopitiwa na Mto Msimbazi, kufuatia malalamiko ya wananchi kwamba baadhi ya shughuli zinazofanyika kwa lengo la kusafisha mto huo zimegeuka kuwa uchimbaji wa mchanga unaochochea mmomonyoko wa ardhi na kuhatarisha miundombinu ya umma na makati wa ya watu.


Akizungumza katika eneo la daraja la Kinyerezi lililopo kata ya Ukonga jijini Dar Es Salaam, Mhe. Kwagilwa amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa katika miundombinu ukiharibiwa kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya vibali vya usafishaji wa mito.


“Madhara mnayoyaona hapa hili daraja siku si nyingi litaondoka. Serikali imeweka mabilioni ya fedha hapa, halafu kuna watu wanatoa vibali vya kusafisha mito na badala ya kusafisha inakuwa ni uchafuzi. ‘Big No’,” amesema Mhe. Kwagilwa.


Ameelekeza taasisi zote zinazohusika kutembelea maeneo yote yaliyotolewa vibali vya kusafisha mito ili kujionea hali halisi na kufanya tathmini ya kina, akisisitiza kuwa lengo la vibali hivyo ni kulinda mazingira na kuboresha mtiririko wa maji, si kufanya biashara ya uchimbaji wa mchanga.


“Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, naelekeza vibali hivi vipitiwe kwa pamoja na wataalamu wa mazingira, mamlaka za mabonde pamoja na halmashauri husika. Uharibifu huu ukiendelea hakuna wa kulaumiana, wote tutaonekana watu wa hovyo,” amesisitiza Mhe. Kwagilwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post