🇹🇿 #Uhamiajiupdates
Na. Mwandishi Wetu, Kigoma
Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma imeendelea kutoa elimu ya masuala ya uhamiaji kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya mpakani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama wa mipaka na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kulinda amani na usalama wa nchi.
Elimu hiyo imetolewa leo, Juni 16, 2026, katika Soko la Ujirani Mwema lililopo Kitongoji cha Kikulazo B, Kijiji cha Kikulazo, Kata ya Rugenge, Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma ambapo waendesha bodaboda wa eneo hilo walipata fursa ya kuelimishwa kuhusu wajibu wao katika kudhibiti uhamiaji haramu na kulinda usalama wa taifa.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Uhamiaji Wilaya ya Kakonko, Mrakibu wa Uhamiaji SI Wilbert Mkoweka, alieleza umuhimu wa wananchi, hususan waendesha bodaboda, kushiriki kikamilifu katika kulinda mipaka ya nchi kwa kutambua wageni wanaoingia na kutoka katika maeneo ya mpakani na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini watu wenye mienendo inayotia shaka.
SI Mkoweka aliwataka waendesha bodaboda kuepuka kusafirisha wahamiaji haramu au watu wasiojulikana bila kujiridhisha kuhusu utambulisho wao. Pia aliwahimiza kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za mapema kuhusu vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Kwa mujibu wa SI Mkoweka, waendesha bodaboda wana nafasi kubwa katika kusaidia mapambano dhidi ya uhalifu na uhamiaji haramu kutokana na kukutana na watu wengi katika shughuli zao za kila siku. Hivyo, aliwahimiza kuwa mstari wa mbele katika kubaini viashiria vya uhalifu na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kwa wakati.
Katika hatua nyingine, SI Mkoweka alipata fursa ya kukutana na maafisa wa Serikali ya Burundi waliokuwa wakitekeleza majukumu yao katika eneo la kizuizi cha Mpaka wa Malenga. Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kubadilishana taarifa kwa wakati kuhusu masuala ya uhamiaji, na mapambano dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka.






Post a Comment