Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania Mkoa wa Dar Es Salaam Mhandisi Lazeck Kyamba katika operesheni ya kuzuia maegesho holela ya malori Mbagala ,amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya malori yanayotumia barabara na kusimama katika eneo la Mbagala Zakiemu kutokana na shughuli mbalimbali za usafirishaji zinazoendelea . Hata hivyo, hali hiyo imekuwa ikichangia msongamano wa magari na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.
Amesema kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakiegesha malori katika maeneo yasiyoruhusiwa, ikiwemo kwenye barabara saidizi (service road), jambo ambalo linaathiri matumizi sahihi ya miundombinu ya barabara na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.
Kutokana na hali hiyo, TANROADS imeendesha operesheni maalum ya kuondoa malori yaliyokuwa yameegeshwa kinyume na taratibu pamoja na kutoa elimu kwa madereva kuhusu umuhimu wa kutumia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya maegesho ya magari makubwa.
Aidha, madereva wamehimizwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani kwa kuepuka kuegesha magari katika maeneo yasiyoruhusiwa, ili kulinda miundombinu ya barabara na kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa barabara.
Meneja amesisitiza kuwa operesheni hizo zitaendelea kufanyika mara kwa mara ili kuhakikisha sheria za matumizi ya barabara zinazingatiwa na kuondoa changamoto zinazotokana na maegesho holela ya malori.
“Lengo letu ni kuhakikisha barabara zinatumika kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa. Tunawaomba madereva wote kushirikiana nasi kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.”








Post a Comment