📌Aandika historia Rais wa kwanza Afrika kutunukiwa Shahada 8 na Vyuo Vikuu vyenye heshima duniani kwa maendeleo makubwa anayoleta nchini mwake._
Na Bwanku M Bwanku.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kuanzia Juni 3 hadi 5, 2026 amefanya ziara ya Kitaifa nchini Urusi kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin.
Kwenye ziara hiyo, Rais Samia alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Putin na kujadili kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa Mataifa haya na maeneo ya uwekezaji huku akihuhutubia Jukwaa la 29 la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg ambalo ni kubwa duniani likikutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali na Wawekezaji wakubwa duniani.
Urusi ni moja ya mataifa 20 tajiri duniani yaliyoendelea katika sekta za viwanda, Kilimo, uhandisi, afya, elimu, sanaa na biashara. Ziara hii itafungua fursa zaidi kwa Taifa.
Pamoja na yote ya kwenye ziara hii, Rais Samia Juni 04, 2026 alitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi- (RUDN University) kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Profesa Oleg Yastrebov kwenye hafla iliyofanyika Chuoni hapo Moscow kutokana na kutambua mchango wake katika Mageuzi ya sekta ya Elimu, juhudi zake za kuimarisha Diplomasia ya Tanzania, pamoja na mchango wake katika kuimarisha hadhi ya Tanzania Kimataifa ikiwemo kupitia sekta ya Utalii.
Kwa kipindi cha takribani miaka 5 kuanzia Machi 19, 2021 alipoapishwa kushika hatamu ya kuongoza Tanzania, tayali Rais Samia ametunukiwa Shahada 8 za heshima na Vyuo Vikuu mbalimbali vinavyoheshimika duniani kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kusukuma maendeleo ya nchi yake kwenye sekta mbalimbali zinazogusa ustawi wa wananchi.
Si jambo linalotokea mara nyingi kwa kiongozi mmoja ndani ya Taifa tena kwa muda mfupi wa miaka 5 kutunukiwa Shahada 8 za Heshima kwa mpigo kwa kutambua mchango wake mkubwa wa maendeleo. Wote tunakumbuka Hayati Rais Magufuli wakati wa uongozi wake wa Awamu ya 5 alitunukiwa mara moja Shahada ya Heshima na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwaka 2019 na Mstaafu Rais wa Awamu ya 4 Jakaya Kikwete pia mwaka 2011 alitunukiwa mara moja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Tayali Novemba 30, 2022 Rais Samia alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa katika masuala ya Binadamu na Sayansi ya Jamii Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Oktoba 10, 2023 akatunukiwa tena Shahada ya heshima ya Udaktari wa Falsafa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru India kwa kusukuma maendeleo ya mtu mmoja mmoja kisha Desemba 28, 2023 akatunukiwa katika Usimamizi wa Utalii na Masoko na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).
Aprili 18, 2024 ikawa zamu ya Shahada ya Heshima ya Uzamivu ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Ankara Uturuki kwa kutambua mageuzi yake ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi na mfumo wake wa 4R.
Juni 03, 2024 ikawa ile ya Udaktari wa Heshima ya Sekta ya Anga ya Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga (Korean Aerospace University) kwa maendeleo aliyoyafanya kwenye maendeleo na sekta ya anga baadae Novemba 24, 2024 ikafuata Shahada ya Uongozi Bora ya Chuo Kikuu cha Mzumbe ikafuata Aprili 11, 2026 kutunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Nasarawa, Keffi nchini Nigeria kwa kutambua mchango wake kama Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia, Afya ya Mama na Mtoto, Taswira nzuri katika masuala ya Uongozi kwa Wanawake Afrika na Kusimamia Masuala ya Biashara hususani kwa Vijana Afrika.
Kwa miaka ya karibuni, anakuwa Rais wa kwanza wa kizazi kipya wa Tanzania kutunukiwa Shahada ya Heshima na Chuo kikubwa chenye heshima kubwa duniani cha Jawaharlal Nehru cha India huku akiandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa Shahada ya Heshima na Chuo hicho na Rais wa 3 pekee baada ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin pamoja ya Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe kutunukiwa na Chuo hicho.
Ndani ya miaka 5, Rais Samia ameshatunukiwa Shahada 8 za Udaktari wa Heshima, tuzo mbalimbali pamoja na kutajwa kwa zaidi ya mara 5 kutoka kwa majarida na taasisi mbalimbali kubwa za kimataifa kwa kutambua kazi yake kubwa anayoifanya kusukuma maendeleo kwenye Taifa lake.
Tayali Jarida maarufu la Avance Media la Ghana lilimtaja kama mmoja wa Wanawake 100 wa Afrika wenye nguvu na ushawishi mkubwa Barani Afrika kabla ya Majarida mengine makubwa yanayosomwa duniani kote kama The Time na Forbes ya Marekani kumtaja pia miongoni mwa Wanawake 100 wenye nguvu ulimwenguni kuanzia mwaka 2022.
Chama Cha Waandishi wa Habari za Miundombinu na Fedha Afrika (MIFA) walimchagua na kumpa Tuzo pia Rais Samia kama Rais aliyefanya mapinduzi makubwa zaidi ya miundombinu Barani Afrika kwa mwaka 2022.
JE, SHAHADA YA HESHIMA INA MAANA GANI? JE, RAIS SAMIA ANASTAHILI MFULULIZO HUU WA SHAHADA ZA HESHIMA ANAZOZIDI KUTUNUKIWA MA VYUO VIKUU MBALIMBALI? JE, NI VIGEZO VIPI VINATUMIKA MPAKA MTU AMA KIONGOZI KUTUNUKIWA SHAHADA YA HESHIMA?.
Shahada ya Heshima ya Falsafa ni Shahada ya juu sana katika elimu inayotolewa na Taasisi ya Elimu ya Juu (Chuo Kikuu) bila ya kumhitaji Mtunukiwa wa Shahada hiyo kufuata utaratibu wa kawaida na uliozoeleka wa kupata Shahada. Utaratibu wa kawaida kupata Shahada ni mtu kuingia darasani kwa muda wa miaka fulani akisoma na kupikwa na baadae akifaulu hutunukiwa Shahada hiyo. Lakini, Shahada hii haimhitaji Mtunukiwa kuingia darasani.
Hii ni Shahada inayotunukiwa ama kutolewa kwa mtu aliyefanya jambo kubwa, la muhimu na lililoacha alama na kubadilisha maisha ya watu kwenye jamii ama Taifa. Jambo hilo linaweza kuwa kwenye sekta ya elimu, kutumia maarifa yake kutatua changamoto kwenye jamii, kulinda na kupigania haki za binadamu n.k.
Kwahiyo, pindi mtu huyo anapofanya jambo ama harakati iliyoleta mabadiliko makubwa kwenye Jamii au Taifa lake, hutunukiwa Shahada hii kama njia ya kutambua mchango na jitihada zake. Jopo la Wasomi na Wanataaluma kwenye Chuo husika kupitia kwa Baraza, Seneti ama Uongozi wa Chuo husika hukaa na kupendekeza utoaji wa Shahada hiyo ya Heshima kwa mtu huyo aliyeonekana kukidhi vigezo kwa mambo yake makubwa aliyoyafanya.
Hivyo, ili mpaka Maprofesa, Wasomi na Wanazuoni wakubaliane kumtunuku mtu Shahada hii ni lazima kweli mtu huyo awe amefanya kazi kubwa inayotambulika na kuacha alama kwenye jamii, iliyoleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi, kijamii, kielimu, kisiasa, kitamaduni n.k.
Tamaduni na asili ya kutoa Shahada hii ya Heshima ilianza miaka ya 1470 kwenye kipindi cha kati cha zama za 'Enlightenment' Barani Ulaya na Marekani kwa Vyuo Vikuu mbalimbali kama Chuo Kikuu cha Oxford na Cambridge kuanza kuandaa utaratibu wa kuwatunuku watu mbalimbali waliokuwa na mchango mkubwa wa kuleta mageuzi katika Jamii.
Mtu wa kwanza kutunukiwa Shahada hii alikuwa Lionel Woodville ambaye alisifika kwa uhodari wake wa kutangaza neno la Mungu na kuuasa ulimwengu kuachana na maasi. Kuanzia hapo sasa, ikawa ndiyo mwanzo wa Shahada hii ya Heshima.
Ikumbukwe, Shahada hii ya Heshima haitolewi tu kienyeji kwa matakwa ya mtu fulani iwe kwa cheo chake ama nguvu ya kifedha bali hufuata utaratibu mrefu wa majadiliano ya kina na jopo la Viongozi wa Chuo husika na Mabaraza yao (Deans).
Chuo Kikuu cha Harvard, moja ya vyuo vikubwa duniani kiliwahi kumtunuku Baba wa Taifa la Afrika Kusini Komredi Nelson Mandela mwaka 1998.
Vyuo vyote 8 hivi vyenye heshima Afrika na duniani vilivyomtunuku Rais Samia Shahada hizi za Heshima wameeleza kwa kina sababu za kumtunuku vikieleza mageuzi makubwa ya maendeleo aliyoyafanya na anayoendelea kuyafanya kwenye utumishi wa umma toka miaka ya 1980 akianza na cheo cha chini kabisa kama Karani wa masjala na zaidi kwenye shughuli za kisiasa alizozianza toka miaka ya 2000.
Hivi vyote vimefanya Mabaraza, Seneti na Wasomi wa Vyuo hivi kumtunuku.
Historia ndefu ya Uongozi iliyojaa utumishi wa kutosha ndani na Nje ya mipaka ya Tanzania akifanya kazi serikalini, kwenye mashirika ya kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's) imechangia pakubwa na alama kubwa kwenye Taifa, akiweka historia ya kuwa Mwanamke wa kwanza kushika hatamu kubwa za Kisiasa kwenye Taifa letu akianzia kuwa Makamu wa Rais 2015-2021 na baadae Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 2021 mpaka sasa huku akiwa pia Mwanamke wa kwanza kuwa Mwenyekiti wa CCM, Chama kinachoongoza Tanzania na moja ya Chama kikubwa na kikongwe Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.
Mageuzi makubwa aliyoyafanya Rais Samia ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake kijamii, kiuchumi, kidiplomasia, uwekezaji, kiutalii na mengine mengi kwenye ustawi wa jamii ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya Elfu 12 na kuondoa kero ya kukaa chini, kuchelewa kujiunga na masomo kwa wanafunzi zaidi ya laki 5 nchi nzima.
Hiyo ni pamoja na kuweka msukumo mpya kwenye ujenzi wa Taifa kwa kuliweka Taifa pamoja baada ya kuonekana kuwa na changamoto kadhaa kwenye eneo hili, kuanzisha maridhiano kwenye uwanja wa siasa kwa kuunda Kikosi kazi Maalum cha kushughulikia changamoto zozote za kisiasa ili Taifa lifanye siasa zenye mlengo wa maendeleo pamoja na kusisitiza Siasa za 4R zikilenga kuja na diplomasia ya kiuchumi ambapo ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake, uwekezaji uliovunja rekodi wa zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 3.5 uliingia Tanzania.
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na kile cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN) vikimtunuku Shahada ya Heshima kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kuinua uchumi wa Tanzania kupitia sekta ya utalii ambapo kuingia kwake aliiamsha sekta ya utalii iliyodorora baada ya kutokea mlipuko wa Janga la Corona ambapo Watalii walikata kabisa, ila kwa jitihada za Filamu kama Royal Tour zikaimarisha utalii kwa kiwango kikubwa hivyo kukuza uchumi wa Taifa.
Rais Samia alikuja na Filamu maalum iliyorekodiwa kwenye vivutio mbalimbali vya Utalii vya Tanzania na Rais Samia Suluhu Hassan kama Mhusika Mkuu (Tour guider) pamoja na Wahusika wengine kwa ajili ya kutangaza utalii wa Tanzania, uwekezaji, utamaduni wa Tanzania na kuiambia dunia ukweli kuhusu vivutio vyote vilivyopo Tanzania na namna Taifa hili la Afrika Mashariki lilivyobarikiwa na fursa nyingi za uwekezaji na biashara ili sasa waje kutalii na kuwekeza Tanzania.
Baada ya Filamu hiyo ya Royal Tour, Taifa lilipata mafanikio makubwa ya kuwavuta Watalii na Wawekezaji wengi zaidi nchini. Kwa mujibu wa serikali, baada ya Watalii kushuka sana mpaka Laki tisa (9) kwasababu ya Janga la Corona, Filamu ya Royal Tour ilifanikiwa kuongeza idadi ya Watalii mpaka kufikia zaidi ya Milioni 1.4 kwa Tanzania Bara ikiwa ni ongezeko la asilimia 57 huku kwa upande wa Zanzibar Watalii wakitoka Laki tatu (3) mpaka Laki tano (5) huku Tanzania kwa mara ya kwanza kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watalii (UNWTO) ikishika nafasi ya pili mwaka 2023 kwa kuingiza Watalii wengi Barani Afrika baada ya Ethiopia.
Mapato ya utalii yakiongezeka mpaka kufikia asilimia 93, hali iliyoongeza fursa za ajira na maendeleo makubwa kwa wananchi.
Hiyo ni pamoja na kazi kubwa aliyoifanya toka akiwa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji kule Zanzibar kutoka mwaka 2005 hadi 2010 ambapo alifanya kazi kubwa ya kusukuma utalii kwa kusafiri mataifa mbalimbali kuwavuta watalii na wawekezaji ambao wengi walifika Zanzibar kujenga hoteli za kisasa na kupaisha zaidi utalii wa Zanzibar.
Haya yote pamoja na mengine ambayo sikuyajumuisha yamevisikuma Vyuo vikuu hivi kumtunuku Rais Samia Suluhu Hassan. Je, kuna ubishi tena kuhusu kustahili kwake? Rais Samia anastahili kutunukiwa Shahada hizi kwa kazi kubwa anayoifanya.
*Makala hii imeandaliwa na Bwanku M Bwanku, Mwandishi wa Habari za Siasa, Uchumi na Maendeleo ambaye pia ni Afisa Tarafa ya Katerero iliyopo Bukoba mkoani Kagera.



Post a Comment