
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Alnason Nguvila amesema kufanyika kwa mafunzo kwa Viongozi na watendaji wa Mkoa, Wilaya, Halmashauri na Taasisi za serikali zilizopo Mkoani Arusha kutawarejesha Viongozi hao kwenye utaratibu unaopaswa kuzingatiwa na kila mmoja ili kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza Mei 28,2026 wakati wa kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua Mafunzo hayo Dkt. Nguvila amebainisha kuwa, mafunzo hayo ya siku mbili, yamewajumuisha Washiriki 230, ambao ni Wakuu Divisheni na Vitengo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Makatibu Tawala Wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Divisheni na vitengo wa Halmashauri zote pamoja na Wakuu wa Taasisi za Umma wa Mkoa wa Arusha.
"Sisi wasaidizi wako tunaamini kuwa tunafanya kazi vizuri na kukusaidia katika kuhakikisha kuwa malengo ya serikali na matarajio ya wananchi wa Mkoa yanafikiwa. Hata hivyo tunaamini inawezekana kuna baadhi ya mambo tunafanya kwa mazoea tu na pengine tunakosea hivyo tunaona ipo haja ya kuwashirikisha wataalamu wengine kutupitisha katika mambo ya msingi kwa lengo la kukumbushana namna itupavyo kutenda na kutimiza wajibu wetu wa kuwatumikia wananchi." Amesema Dkt. Nguvila.
Kulingana na Dkt. Nguvila kufanya kazi kwa mazoea kunasababisha kukosea, kukiuka miiko ya maadili ya kazi, kushusha ari ya kazi, kushusha heshima ya taasisi, kuvuka mipaka ya mamlaka na madaraka pamoja na kuchelewesha huduma kwa wananchi.
Katibu Tawala huyo amesisitiza kuwa ni matarajio yake kwamba mafunzo hayo yataendelea hadi ngazi ya Maafisa tarafa, watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijiji na Mitaa, akisema ni matamanio yake kuwa Arusha iwe ya lugha moja kuanzia ngazi ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hadi kwa Mtendaji wa Kijiji na Mtaa

Post a Comment