SERIKALI YAIMARISHA UTOAJI ELIMU KWA WANAWAKE KUHUSU TEZI YA SHINGO



Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wanawake kuhusu magonjwa ya tezi ya shingo (thyroid) ili kuongeza uelewa wa chanzo, dalili na njia za kinga ya ugonjwa huo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, leo Aprili 15, 2026 bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Mariam Anzuruni Mungula, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali katika kutoa elimu kwa wanawake kuhusu magonjwa hayo yanayoweza kuathiri ukomo wa hedhi (perimenopause).

Dkt. Samizi amesema ugonjwa wa tezi ya shingo ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, ambapo tafiti zinaonesha kuwa wanawake wako katika hatari kubwa zaidi ya kuathirika, huku wagonjwa 9 kati ya 10 wakiwa ni wanawake na wanawake 12 kati ya 100 wakiwa katika hatari ya kupata ugonjwa huo.

Amesema visababishi vya ugonjwa huo ni pamoja na kushambuliwa kwa tezi na kinga ya mwili (autoimmune), mabadiliko ya homoni ikiwemo estrogeni, projesteroni na homoni za tezi, upungufu wa madini joto mwilini, urithi wa kifamilia, umri zaidi ya miaka 60 pamoja na msongo wa mawazo na mtindo wa maisha.

Kuhusu hatua zinazochukuliwa, amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo redio, runinga, mitandao ya kijamii, mabango na vipeperushi kuhusu chanzo, dalili na kinga ya ugonjwa huo.

Aidha, Serikali inaendelea kusimamia matumizi ya chumvi yenye madini joto, kuimarisha kampeni za lishe bora pamoja na kuhamasisha matumizi ya vyakula vyenye madini hayo muhimu.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za uchunguzi, vipimo na matibabu ya magonjwa ya tezi katika ngazi zote za utoaji huduma za afya, sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya ili waweze kutambua mapema na kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa.

Serikali imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu na huduma za afya zinawafikia wananchi kwa lengo la kupunguza athari za magonjwa ya tezi ya shingo nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post