Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, amesisitiza umuhimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha utendaji wa kazi na kufungua fursa mbalimbali za maendeleo, hasa kwa vijana wa kike.
Akizungumza katika Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana katika TEHAMA, Dkt Mkama amesema kuwa nchi nyingi duniani zimeendelea kuhamasisha wasichana kusoma masomo ya TEHAMA ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali.
Ameeleza kuwa TEHAMA inamwezesha kijana kufanikiwa katika masomo, ajira pamoja na ubunifu wa fursa mpya.
Aidha, ametoa wito kwa wakuu wa shule na vyuo nchini kuanzisha klabu za kidigitali zitakazosaidia kuwaandaa wanafunzi, hususan wasichana, kukabiliana na ushindani wa kimataifa katika sekta ya teknolojia.
Dkt. Mkama amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo endelevu wa kuwafuatilia na kuwaendeleza washindi wa mashindano ya TEHAMA, badala ya kuwaacha baada ya kupokea zawadi, ili kuhakikisha vipaji vyao vinaendelea kukuzwa.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Jabiri Bakari, amesema kuwa matumizi ya Akili Bandia (AI) yameongezeka kwa kasi duniani kutokana na maendeleo ya teknolojia, ikiwemo uwezo mkubwa wa kukusanya na kuchakata taarifa.
Amebainisha kuwa AI si teknolojia mpya, bali ilianza tangu miaka ya 1950, lakini kwa sasa imepata nguvu zaidi na imekuwa sehemu ya mifumo mingi ya kidigitali, ikiwemo huduma za simu.
Mhandisi Bakari amesema wasichana wana nafasi kubwa katika sekta ya TEHAMA, hasa katika kubuni suluhisho na ubunifu wa kiteknolojia, na hivyo wanapaswa kuchangamkia fursa za kujifunza ili kuwa sehemu ya kizazi cha kidigitali.
Wasiliana na Habarika24 kupitia WhatsApp kwa namba+255784747478


Post a Comment