MAKAMU WA RAIS, BALOZI DKT. EMMANUEL NCHIMBI AONGOZA MAADHIMISHO YA KILELE CHA WIKI YA MAJI KWA MWAKA 2026 NA SIKU YA MAJI DUNIANI

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa Mamlaka zinazohusika pamoja na Watanzania kwa ujumla kuweka kipaumbele katika utunzaji na ulinzi wa vya vyanzo vya maji ili kuweza kurithisha kizazi kijacho nchi inayofaa kuishi.

Makamu wa Rais ametoa wito huo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Maji kwa Mwaka 2026 na Siku ya Maji Duniani iliyofanyika katika Viwanja vya Mkwawa mkoani Morogoro leo tarehe 22 Machi 2026. Amesema ni lazima kuangalia sana umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati ambao unaangalia kuvitunza na kuongeza vyanzo vya maji.

Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa rai kwa Wizara na Taasisi zote za Umma nchini kujenga mtandao wa ushirikiano katika kuzikabili kuzitatua na kurekebisha changamoto za maji ili dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Taifa lilioondokana na changamoto za maji safi na salama iweze kufanikiwa.

Pia amesema, ni vema kwa Mamlaka za Maji nchini kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kukuza sekta ya maji. Ameipongeza Mamlaka ya Maji Tanga kwa kutumia mfumo wa Hati fungani katika kugharamia miradi ya maji inayotekelezwa mkoani humo. Makamu wa Rais amesema kila mtanzania anapaswa kuona wajibu wa utunzaji wa mazingira.

Vilevile, Makamu wa Rais amesema, Sekta binafsi ni mdau muhimu katika kufanikisha miradi ya maji kwa maendeleo ya sekta hiyo. Ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya maji kutambua kwamba maji ni muhimu na hitaji la kila mwanadamu hivyo ni vema kuendelea kushirikiana.

Makamu wa Rais, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji unafanikiwa kikamilifu kwani kufanikiwa kwake ndio kuondokana na tatizo la maji nchini. Amewasihi Wizara ya Maji kuhakikisha wanafanikisha ufungaji wa mita katika maeneo ya matumizi ya maji ili kuepusha upotevu wa maji lakini pia kufanya watu wanaotumia maji kuwajibika.

Post a Comment

Previous Post Next Post