
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa yaliopo Kikombo jijini Dodoma.
*DKT. SAMIA: JESHI EPUKENI MIENENDO MIBAYA, WANANCHI WANA IMANI NANYI*
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewakumbusha wanajeshi nchini kuwa nguvu ya kweli ya jeshi haipo kwenye majengo ya kisasa wala zana za kivita, bali katika moyo wa kizalendo na utii kwa Katiba.
Akihitimisha hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa yaliyopo Kikombo jijini Dodoma leo, Februari 24, 2026, Rais Samia amesisitiza kuwa uaminifu kwa taifa na utii kwa mamlaka zilizowekwa kikatiba ndizo nguzo zinazolifanya jeshi liheshimike ndani na nje ya mipaka ya nchi.
Rais Samia amewasihi makamanda na wapiganaji hao kuishi kulingana na viapo vyao na kuepuka mienendo inayoweza kuchafua taswira ya jeshi ambayo Watanzania wameijengea imani kubwa.
Pamoja na kutoa maelekezo kwa wanajeshi, Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania wote kutekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kulinda amani na utulivu. Amesema amani ya nchi si jukumu la wenye sare pekee, bali ni dhamana ya kila mwananchi katika kuhakikisha taifa linabaki salama kwa ajili ya maendeleo.
TANZANIA YAJIVUNIA KUKUA KIUCHUMI KWASABABU YA AMANI
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa uimara wa ulinzi na amani ndio msingi mkuu ulioifikisha Tanzania katika daraja la juu la ukuaji wa uchumi duniani.
Akizungumza leo, Februari 24, 2026, wakati wa uzinduzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa yaliyopo Kikombo, mkoani Dodoma, Rais Samia amebainisha kuwa hakuna maendeleo wala uwekezaji unaoweza kustawi bila ulinzi thabiti.
Rais Samia amehusisha mafanikio ya kijeshi na tathmini ya hivi karibuni ya shirika bobezi la kiuchumi duniani, Moody’s, ambalo limeipa Tanzania daraja la B1, kiwango ambacho kinavutia wawekezaji wakubwa.
Rais ameweka wazi kuwa serikali itaendelea kuwekeza kwa nguvu katika sekta ya ulinzi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi. Amesema uwekezaji huo ni suala lisiloepukika kwani taifa lolote linalotaka kuheshimiwa duniani lazima liwe na taasisi imara za kulinda uhuru, mipaka, na rasilimali zake.
#KaziNaUtuTunasongaMbele
#TabasamuLaUtu
#maendeleoendelevu
#nchiyetukwanza

Post a Comment