Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Mashaka Biteko amezindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2025-2029.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Mpango huo Agosti 19, 2025 uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani (TPTC) kilichopo Kunduchi mkoani Dar Es Salaam, Dkt. Biteko amezitaka Wizara na Taasisi za Serikali na Wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha wanatenga Bajeti ya utekelezaji wa Mpango huo ili kutimiza malengo yake.
"Naomba nitoe rai kwa Wizara zote zenye dhamana ya agenda hii; Tanzania Bara na Zanzibar; mkasimamie na kutekeleza mpango huu kama ilivyokusudiwa ili kufikia malengo stahiki" amesema Dkt. Biteko
Aidha Dkt. Biteko amesema katika utekelezaji wa Mpango huo amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wakiwa Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye maeneo yao kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Mpango huo kwa kushirikiana na wadau waliopo.
"Niwaombe kuhakikisha kuwa mnatoa elimu na kuhamasisha, ushiriki wa wanawake na wanaume katika hatua zote za kuzuia, kutatua migogoro na ujenzi wa amani, ulinzi na usalama." amesisitiza Dkt. Biteko
Akitoa salamu Wizara Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema katika kuandaa Mpango huo, uainishaji wa maeneo mahsusi ya vipaumbele vya Mpango umezingatia maudhui ya Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Post a Comment